Friday, March 8, 2013

TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUFUATIA SHAMBULIO LA KIKATILI DHIDI YA MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI BW. ABSALOM KIB[ --

Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu ambao ni kusanyiko la zaidi ya asasi 70 za kiraia zinazotetea haki za binadamu (THRD-Coalition) , kwa kushirikiana na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habati Tanzania (UTPC) pamoja na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini kwa Africa (MISA-Tan) tunalaani vikali shambulio la kinyama alilofanyiwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda usiku wa kuamkia jana Jumatano tarehe 6 Machi, 2013.
Bw. Kibanda alivamiwa wakati alipokuwa anarudi nyumbani kwake Mbezi juu. Watu hao walimteka na kisha wakamtesa kinyama kwa kumng’oa meno, kucha, kidole na kuliharibu vibaya sana jicho la upande wa kushoto. Huu ni ukatili, unyama dhidi ya utu wa binadamu. Baada ya kutekeleza azma yao walimtupa umbali wa mita 30 toka alipokuwa amepaki gari lake.
Uchunguzi tulioufanya bado haujatujapatia habari za undani zaidi na za uhakika wa tukio hilo. Lakini kwa taarifa za awali kwa asilimia kubwa linahusiana na kazi yake ya utetezi wa haki za binadamu kupitia katika taaluma yake ya uandishi wa habari. Hii ni kwa sababu pia tayari alishafunguliwa kesi mahakamani inayohusu uandishi wake.
Tunasema hivyo kwa sababu vitisho dhidi ya wanahabari na watetetezi wengine wa haki za binadamu vinataka kuzoeleka sasa hapa nchini jambo ambalo halikuwapo katika miaka ya nyuma. Takribani ndani ya miezi 10 sasa zaidi ya watetezi wa haki za binadamu 10 wakiwamo waandishi wa habari wameshajeruhiwa, wamepata vitisho au kuuwawa.
Matukio haya yanaashiria lengo la kutaka kuzima sauti za watetezi wa wanyonge kwa visingizio mbali mbali huku matukio ya aina hii wakati mwingine yakipewa sura tofauti tofauti ikiwamo uhalifu wa kawaida, visa vya kudhulumiana na visasi vya kimapenzi. Ni dhahiri wanaofanya hivyo wana malengo mabaya ya kuchafua jina na taswira nzuri ya nchi yetu katika Jamii ya Kimataifa kwa malengo binafsi.
Wakati tukio hili linapojitokeza sasa, bado Mtandao wetu unafuatilia kwa karibu kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi na mazingira ya kukamatwa na kuhojiwa kwa waandishi wa gazeti la Tanzania Daima kulikofanywa na Jeshi la Polisi hivi karibuni kwa kile kilichoitwa kwamba ni kuandika habari za uchochezi.
Tunajiulia je nini Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla wamelifanya kuhusiana na kutekwa na kuteswa kwa Dkt Ulimboka zaidi ya Kulifungia Mwanahalisi ambalo lilijitoa mhanga kuchunguza suala hili? Ndugu Kibanda katekwa na kufanyiwa kile kile alichofanyiwa Ulimboka, Je tume iliyoundwa itaanzia kwa Ulimboka ama itarukia moja kwa moja tukio hili ambalo ni muendelezo wa matukio lukuki dhidi ya watetezi wa haki na waandishi kwa ujumla.
Hatupendi kuingilia wala kukwamisha utendaji kazi wa jeshi hilo, lakini pia hatupendi wanahabari na watetezi wengine wafanye kazi yao katika mazingira ya woga. Tunaamini kwamba zipo njia muafaka zaidi za kushughulikia masuala yanayohusu taaluma ya habari. Kwa mfano lipo Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambalo linajukumu ya kusuluhisha migogoro inayohusiana na taaluma hiyo na iwapo itashindikana basi mhusika au wahusika bado wanakuwa na nafasi ya kwenda mahakamani.
Kinachoshangaza ni kuona kwamba Jeshi la Polisi limefikia mahali pa kwenda kuwakamata waandishi na wahariri wa Tanzania Daima ndani ya chumba chao cha habari na kuwakagua hadi katika makazi yao na kuchukua nyaraka kadhaa kama ilivyotokea kwaa Bw. Josephat Isango.
Hali hiyo ya mahojiano ya kushtukiza na kuogofya imefanyika pia kwa wahariri Charles Misango na Edson Kamukara wote wa gazeti hilo, ambapo hatima yao bado haifahamiki mpaka sasa. Hali hii inaweza kusababisha woga kwa wanataaluma wengine na hivyo kuleta athari kubwa katika sekta ya habari nchini.
Waandishi hao kwa sasa wanaishi kwa woga. Je kwanini tufikie hatua hii ya kufanya wenzetu waishi kwa hofu kama swala kwenye mbuga iliiyojaa simba?. Je ulinzi wa vyombo vya usalama upo kwa ajili ya nani? Kwanini wengine wauawe, watekwe, wateswe na kudhalilishwa huku vyombo vya usalama vikichukulia ni jambo la kawaida na kutupiana mpira?
Rai Yetu
1. Tunawataka watu wote wanaotumika au wanaoendeleza wimbi la mashambulizi kwa wanahabari na watetezi wote wa haki za binadamu kwa ujumla, waache kufanya hivyo kwani wataliingiza nchi katika machafuko makubwa.
2. Tunalisihi Jeshi la Polisi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubeba jukumu lao la kuhakikisha usalama wa watetezi wa haki za binadamu, na raia na watu wote waliomo ndani ya mipaka ya nchi hii kwa ujumla bila ubaguzi.
3. Tunaomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini wahusika wa mtindo huu wa kuteka kutesa na kutelekeza kwani tukio hili la Kibanda linashabihiana kwa kiwango kikubwa na lile la Dkt Stephen Ulimboka.
4. Tunaiomba jamii yote ya watu waliostaarabika, makundi mbalimbali kutuunga mkono katika jitihada zetu la kupigania amani, haki na uhuru kwa watu wote hasa hasa watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari.
5. Tunawakumbushia waandishi wa habari kujitahidi kupata mafunzo ya usalama ambayo yanaratibiwa na kutolewa na Mtandao huu wa watetezi.
6. Vyombo vyote vya habari na waandishi kwa ujumla wazidi kuwa pamoja katika kipindi hiki kigumu cha kuelekea chaguzi za serikali za mitaa mwakani pamoja na uchaguzi mkuu 2015. Pia wajieupushe na makundi ya kisiasa ili kujiweka vizuri katika kufanya kazi zao kwa kufuata misingi ya taaluma zao.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
Imeletwa kwenu na
Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu Tanzania (THRD-Coalition)
K.n.y Watetezi Wote wa Haki za Binadamu Tanzania

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA