Sunday, March 3, 2013

BAADA YA FBI KUINGIA NCHINI, WATUHUMIWA WALIOMUUA PADRE MUSHI WAANZA KUKAMATWA

K
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi  Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa alithibitisha kwamba jeshi lake limekuwa likishirikiana na FBI katika upelelezi huo na kwamba idadi ya waliokamatwa imeongezeka.
UJIO wa Askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) nchini na kuanza kufanya kazi, umewezesha kuanza kunaswa kwa baadhi ya watu, wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya Padre Evarist Mushi (55) wa Kanisa Katoliki Unguja, visiwani Zanzibar.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumamosi  Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa alithibitisha kwamba jeshi lake limekuwa likishirikiana na FBI katika upelelezi huo na kwamba idadi ya waliokamatwa imeongezeka.
“Ni kweli tumekuwa tukishirikiana na FBI katika upelelezi ili kuhakikisha kuwa, wahusika wa tukio la kuuawa kwa Padri Mushi wanakamatwa. Hii itasaidia kupunguza vitendo vinavyohusishwa na matukio ya kigaidi yakiwamo mauaji,”alisema Kamishna Musa.
Alisema kuwa hilo linafanyika ili kuhakikisha kuwa, zoezi la kuwakamata wahusika wa uhalifu huo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa, jambo alilosema linaweza kupunguza matukio ya mauaji.

Alibainisha kwamba hadi sasa kuna ongezeko la idadi ya watu waliokamatwa na kwamba watu hao wanaendelea kuhojiwa, huku wengine wakishikiliwa kwa sababu maalumu.
Kamishna Musa alifafanua kuwa  kutokana na zoezi hilo watu watakaobainika kuhusika na mauaji hayo watafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua zaidi.
Padri Evaristus Mushi aliuawa Februari 17, mwaka huu kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa, wakati akienda kuongoza misa katika Kanisa la Mtakatifu Theresia la Beit el Rass.
Juzi, Kamishna Musa aliliambia Gazeti hili kwa njia ya simu kwamba wapelelezi wa kigeni wamewasili Zanzibar kufanya uchunguzi wa kuwabaini waliomuua kwa kumpiga risasi, Padri Evarist Mushi.

Alisema kuwa wapelelezi hao tayari wameanza kazi hiyo kushirikiana na wenzao wa Tanzania kuwasaka wauaji wa padri huyo aliyepigwa risasi Februari 17, mwaka huu.
“Wapelelezi kutoka nje wamefika na wapo kazini,” alisema Kamishna Mussa bila ya kutaja wanatoka nchi gani.

Pia Kamishna Mussa hakutaka kueleza ni lini wapelelezi hao walifika Zanzibar na idadi yao kwa maelezo kwamba hizo ni siri za polisi na kwamba zikivuja, zitaingilia uchunguzi wanaoufanya.
Hata hivyo, vyanzo vya ndani ya Serikali, vililithibitishia Mwananchi kuwa FBI walikuwa wameanza kuwasaka wauaji wa Padri Mushi.

Kutua kwa wapelelezi hao wa Marekani kunafuatia kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za rambirambi baada ya mauaji ya Padri Mushi, kuwa amewaagiza polisi kutumia nguvu zake zote pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya usalama vya ndani na mashirika ya upelelezi ya nchi rafiki katika kufanya uchunguzi wa mauaji hayo.


Awali, akitoa tamko la Serikali na kueleza kuwa Rais Kikwete ameidhinisha Serikali kugharamia wapelelezi kutoka nje, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alihusisha tukio hilo na vitendo vya ugaidi.

Ujio huo wa FBI pia unaweza kuhusishwa moja kwa moja na dhamira iliyoonyeshwa mapema na Serikali ya Marekani kuwa ipo tayari kusaidia upelelezi wa mauaji hayo.
Dhamira hiyo ilibainishwa katika salamu za rambirambi za kifo hicho zilizotolewa na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt.
Vyanzo mbalimbali kutoka ndani ya Serikali vimeeleza kuwa kabla ya kuanza kwa operesheni hiyo, maofisa wa FBI walifanya mazungumzo na Waziri Nchimbi na viongozi wengine wa Serikali kwa ajili ya kuangalia namna watakavyofanya shughuli hiyo.

1 comment:

  1. Gambling apps for Android and iOS - The JTM Hub
    Gambling 토토사이트 apps for Android and iOS is now 여주 출장샵 available for the Google Play store, with the 춘천 출장안마 latest 김천 출장안마 mobile apps and services from the developer. Android users 속초 출장마사지 can

    ReplyDelete

TOA MAONI YAKO HAPA