Monday, January 28, 2013

BREAKING NEWS: LULU APEWA DHAMANA LEO


Habari zilizotufikia hivi punde zinadai kuwa Mahakama kuu ya Tanzania imemwachia kwa dhamana msanii wa filamu nchini Tanzania, Elizabeth Michael aka Lulu aliyekuwa mahabusu katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam.

Lulu alifikishwa mahakamani akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba, ambaye hata hivyo baadaye alibadilishiwa kesi na kushitakiwa kwa kuua bila kukusudia.

Msanii huyo ameachiwa huku akipewa masharti ya kuacha Hati ya Kusafiria Mahakamani, kuripoti Mahakamani kila tarehe mosi, pamoja na wadhamini wawili waliotoa milioni 20 mmoja.
Kwa wiki kadhaa sasa, baadhi ya watu wamekuwa wakisikika wakiomba dua njema kwa msanii huyo ili aweze kuachiwa kwa dhamana na kufuatilia kesi yake akiwa nje na familia yake.
Lulu aliwasilisha mahakamani hapo maombi ya dhamana, kupitia kwa jopo la mawakili wake, linaloongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala, Fulgence Masawe wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Awali, maombi hayo ya dhamana yaliwasilishwa mahakamani hapo kwa hati ya dharura na kusikilizwa na jaji Zainabu Muruke.
Mara baada ya tukio la mauaji ya Kanumba kutokea, kesi ya msanii huyo ilifunguliwa katika Mahakama ya Kisutu ili kukamilisha hatua za awali, hasa masuala yote ya kisheria, upelelezi na kushtakiwa kwa mauaji ya kuua bila kukusudia kwa kupitia Kifungi cha 196.

Kesi ya Lulu yenye namba 125, jalada lake lilifungwa na kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa kuwa ndiyo yenye uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Mara baada ya kufika mahakamani hapa leo asubuhi, dalili njema za kuachiwa kwa msanii zilianza kujitokeza hasa baada ya dhamana yake kuwa wazi, ikiwa ni kutokana na hoja zilizokuwa zinajadiliwa mahakamani hapo.
Katika mitandao ya kijamii, ikiwamo facebook, baadhi ya watu walionekana wakipost habari na picha mbalimbali za msanii huyo zikionyesha dhahiri kumuombea mema ili atoke na kuendelea na maisha yake wakati kesi hiyo inaendelea.
Lulu ni miongoni mwa wasanii wa kike wenye mvuto mkubwa katika jamii, huku uwezo wake na umahiri wake wa uigizaji ukiacha watu midomo wazi.
Umaarufu wa Lulu ulitokea tangu mdogo akiigiza katika kundi la Kaole Sanaa Group, akicheza kama mt0to hadi kufikia kuwa msichana na mwenye mvuto miongoni mwa mabinti wa filamu Tanzania.
Bila shaka habari za kuachiwa kwa dhamana kwa msanii huyo zitakuwa njema kwa siku ya leo kwa mashabiki na wadau wote wa filamu Tanzania.

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA