Wednesday, February 27, 2013

KAMA HUKUPATA NAFASI YA KUSOMA WARAKA WA MH LEMA KWA RAIS KIKWETE HUHUSU UDINI USOME HAPA



Mh Rais Nakusalimu,

Wakati mwingine unapaswa kupewa pole na kuombewa na kufanyiwa dua kwani wewe ndie unatumikia ofisi kubwa kuliko zote Nchini na wakati huo huo unapaswa kupewa hongera kufikia malengo yako hayo ya kutumikia ofisi kubwa na ya Heshima kuliko zote Nchini , nimekuwa nikitafakari sana suala la Udini katika Taifa letu na huko Nyuma mwaka jana nilikuandikia pia waraka kuonya na kukumbusha hatua mathubuti kabla mambo hayajaaribika sijui kama ulisoma lakini naamini Usalama wa Taifa ambao siku hizi wanatumikia CCM watakuwa walisoma na Nape na wenzake pia walipata fursa ya kuusoma . Mh Rais katika waraka hule nilisema hivi “ Mh Rais Taifa linahitaji Tiba “ siwezi leo kuandika kile nilichosema katika waraka ule ila niliweza kubashiri sumu ya udini inayoendelea katika Taifa lako na langu, Mh Rais , ukweli nakwambia ukifanya mchezo kidogo sana Taifa hili linapotea likiwa mikononi mwako kwani hali ya Nchi sio nzuri hata kidogo na watu waliokuwa wanaishi kwa umoja na upendo sasa wanaanza kutafuta mbinu za kugombana na kuuwana.

Mh Rais, Siasa ya Udini na Ukanda makusudi yake yalikuwa kudhoofisha vyama vya upinzani na yalifanikiwa kwa baadhi ya vyama kudhoofishwa sana na mkakati huo unaendelea dhidi ya Chadema lakini kinachosikitisha ni kuwa wale waliobuni mkakati huo walishindwa kutafakari au kuona madhara yake mbele .

Mh Rais, mkakati wa kudhoofisha Chama cha Siasa kwa Udini na Ukanda hauishi tu kuangamiza hicho Chama bali kuwagawa Watu na Taifa kwa Ujumla , Mtu anapojaribu kusema Chadema ni Chama cha Wakristo kimsingi matamshi hayo hayaangamizi Chadema tu bali yanagawa Watu kwa matabaka ya Udini wao na na kufanya Dini moja iamini kuwa Dini nyingine ni mbaya na hivyo mpango huo unafanya Watu waanze kutazamana kwa Udini na Ukabila na matokeo yake ndiyo haya tunaanza kuyaona leo . Mh Rais, Taifa linahitaji tiba , Hivi karibuni Waziri Mkuu alienda Geita kwenye mgogoro wa Waisilamu na Wakristo na niliona mawazo ya Waziri Mkuu kwenye vyombo vya habari na kwa kweli nilisikitika kwa busara zile zilizokuwa zimejaa hofu kubwa . Tatizo lile lilianza na nani kati ya Mkristo na Muislamu anayepaswa kuchinja?


Mh Rais , Nilipoona jambo hili nilianza kujiuliza maswali mengi sana, kwanza , umakini huu kwa pande zote mbili juu ya jambo hili umeletwa na nini na nani? Kwani yako mambo mengi yaliyokatazwa na Biblia na Msaafu ambayo watu wote wa dini hizi mbili wamekataa kuyatii au kuyafuata , kwa mfano waislamu na wakristo vijana kwa wazee wanakunywa pombe pamoja baadhi yao kujenga mahusiano hata ya kimapenzi yasiyo rasmi bila hata kufuata utaratibu wa Msaafu wala Biblia lakini hapa hutaona ugomvi mkubwa sana japokuwa ni masuala yanayo mkera na kumuudhi mwenyezi Mungu sana.

Mh Rais , ndio maana katika suala hili la nani achinje kati ya Muislamu na Mkristo niliposikia maafa yake nikakumbuka waraka niliokuandikia mwaka jana kuhusu choko choko za Udini ambazo zimeanza

kuleta maafa ambazo Mwanzilishi wake ni CCM .


Mh Rais Chama chako unachokiongoza , Team yako imekuwa ikifanya sana propaganda hizi za, Udini ,
Ukabila , na Ukanda usiku na mchana , lakini nimekuwa nikikerwa sana na Jinsi kabila la Wachaga linavyochukuliwa katika propaganda hizi na wanaofanya hivyo asilimia kubwa ni mashemeji wa Wachaga na mimi najiuliza wanaweza vipi kufanya Siasa za Ukanda na Ukabila wakati wao wenyewe ni familia moja ?
Kwa mfano , Mh Mwigulu Nchemba , Mh David Mathayo , Mh January Makamba , Mh Benjamin Mkapa , Mh Fredrik Sumaye , Mh Theo , Mh Dr Faustin Ndungulile , Mh Prof Ibrahimu Lipumba , Pro Mahalu , Mh Dr Hamis Kigwangala , Mh John Mgufuli , Mh Sospeter Muhongo , Mh Jaji Warioba, Idd Simba, Mh Salmin Amour , na wengine wengi wote hawa wameoa Kilimanjaro . Sasa unajiuliza hawa wote ni Viongozi ndani ya CCM na wengine ndio mabingwa wa kufanya Siasa za Udini na Ukanda , je wake zao ndani ya nyumba wanajisikiaje wanapoona waume zao wanatukana kabila za ndugu zao kwa sababu ya Siasa ? Hii ni hatari kubwa Mh Rais kama kuchinja ni suala zito kiasi hicho katika Imani ya Kiislamu na pia ni neno kutoka katika Kitabu cha Imani yao basi ni haki na kweli kuwa wao wanapaswa kuchinja kwa Imani ya Dini yao na wala wasilazimishwe kumkosea Mungu wao kwani hakuna maarifa na Busara inayozidi imani, lakini vile vile Wakristo wasilazimishwe kushiriki Ibada ambayo sio yao. Waislamu kama wanaamini kuwa wao kuchinja ndio jambo lililoamrishwa katika vitabu vyao basi sasa Jambo hilo liheshimiwe na kutafutiwa utaratibu na vile vile Wakristo wasipuuzwe kugoma kushiriki jambo ambalo kwa wengine lina sura ya Imani.
Nini Kifanyike?

Kwanza Chama chako na Viongozi wake uwakanye na kuwashauri mara moja kabisa kuacha propaganda za udini na ukanda , kwani katika hili hakuna namna Nchi inaweza kubaki salama , kwani hizo choko choko hazitokani na nia mbaya ya Waislamu na Wakristo bali ni siasa chafu iliyopandikizwa ili kuangamiza vyama vya Siasa na sasa imekwenda zaidi na imeanza kuwatesa wakati ambao Nchi ina matatizo mengi , Kwa mfano Chadema tulipoandama Arusha kupinga Uchaguzi wa Meya feki , Kiongozi mmoja wa Mkoa wa CCM hapa Arusha , alinukuliwa na vyombo vya habari akidai tunafanya maandamano hayo kwa sababu za Udini na ndio maana hatumtaki Meya , lakini kitu cha kushangaza huyu Meya Feki ni Mkristo tena Mchaga Kabila langu , lakini niliambiwa na tunampinga na Maaskofu wanampinga kwa sababu Chadema ni Chama cha Udini ‘ sasa najiuliza kama Meya huyu Feki ni Mchaga na ni Mkristo je hayo madai ya kijinga yanatoka wapi ? Kama Ukristo ni ajenda kubwa kwetu kwani nini tulimpinga sasa ? Huu ni mfano mmoja iko mingi sana inayoashiria mkakati wa makusudi wa kuangamiza Chadema na huku mkisahau kuwa maliangamiza Taifa , na ndio Mkuu wa Mkoa wa Arusha alipokuja tu alidai kuwa amekuja kupambana na Chadema na Wachaga , ila nimuhakikishie hataweza na asijaribu kamwe na mikutano ambayo amekuwa akiifanya aiche mara moja .
Pili, Mh Rais, ninaamini kuwa wewe umesafiri Nchi mbali mbali kuliko mimi , Ukienda Marekani , Spain , Brazil , China , Hong Kong , UK, Italy , Sweden, Botswana , Namibia , South Afrika , Zimbabwe na Nchi nyiongi utaona Maduka au Mabucha ya Nyama yameandikwa (Halal ) au unanua bidhaa yeyote ya aina ya Nyama na kukuta imeandikwa “Halal” na ni ustarabu kwamba bidhaa hiyo machinjio yake yamezingatia maadili ya Dini ya Kiislamu na Waislamu wenye Imani thabiti na Imani yao hapo ndipo watakapofanya manunuzi yao katika bidhaa hiyo ya aina ya Nyama. Lakini maeneno hayo hayo unaweza kupata nyama katika maduka mbali mbali yasiozingatia utaratibu huo na kwa hivyo watu wasiojali sana masuala ya Imani wala hawatasumbuka kuuliza na kusoma kama Nyama hiyo imezingatia masuala ya matakwa ya Imani Fulani.

Hivyo, Mh Rais, nafikiri ni vyema utaratibu huu ukaletwa hapa kwetu ili tuonyeshe Kujali Imani ya Waislamu katika Jambo hili ambalo limekuwa kwazo katika Jamii hizi mbili kubwa na kama ufumbuzi wake hautakuwa kuzingatia hili basi tarajia uchungu kuendelea kutembea kwenye vifua vya watu bila kusema na siku moja hali inaweza kuwa mbaya na tukapoteza Taifa. Mh Rais, naiona hofu isiyokuwa ya kweli ya Mh Waziri Mkuu kuwa tukiruhusu hilo kuwa Wakristo na Waislamu wataweza kutengana kwenye mambo mengine mengi haswa katika Biashara na mambo mengine , kitu ambacho nasema sio kweli kwani , Sukari ,Mchele , Soda na Juisi na bidhaa nyingi hazina makatazo na maelekezo katika Imani , Mfano kila Mkristo anajua kuwa Mwislamu hatumi Nguruwe na Nguruwe kwa mwislamu ni haramu na hivyo Mkristo hawezi kupika Nguruwe na huku akijua kuwa wageni wake siku hiyo ni Waislamu.

Kwa hiyo hofu ya kuligawa Taifa kwa kurusu jambo hili haliwezi kutokea kwani ni miiko ya Kiimani ambayo pande zote zinapaswa kuheshimiana ili upande mmoja usione umekandamizwa na kupuuzwa , na hofu ya kibiashara inayoweza kutokea katika suala hili inapaswa kupuuzwa kwani IMANI ni zaidi ya Biashara japokuwa sioni jambo hili likitokea . Mh Rais, nisikuchoshe sana, lakini haya ni maoni yangu na Mke wangu na sio Chama changu tumeamka leo Asubuhi tukasema tukuandikie tena kwani wewe ni Mkuu wa Nchi , Najua unaweza kuwa busy sana kusoma waraka huu mrefu ila najua Mwigulu na Nape lazima wausome na Rizwan pia hivyo niwaombe wakufikishe ujumbe huu kwa niaba ya familia yangu. Mh Rais , We are pressed on every side by troubles, but not crushed and broken. We are perplexed because we don,t know why things happen as they do . But we don’t give up and quit, we are hunted down BUT God never abandons Us, We get knocked down BUT we get up again and keep going. The root of life need commitment and there’s a lot of suffer to get at the Climax. Don’t Give Up Mr President please, Help our Country now.

Godbless Jonathan Lema

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO HAPA